Maisha ya Mtakatifu Bonaventura – Askofu na Mwalimu wa Kanisa

(Kumbukumbu: 15 Julai)

Leo Kanisa Linamkumbuka na Kumheshimu Mtakatifu Bonaventura Askofu na Mwalimu wa Kanisa 

Mtakatifu Bonaventura

 

 

Jina la Kiasili na Mahali Alipozaliwa

Mtakatifu Bonaventura alizaliwa mwaka 1218 huko Bagnoregio, katika mkoa wa Toskana nchini
Italia. Wazazi wake walimpa jina la Yohane alipobatizwa. Tokea utoto wake,
maisha yake yalionekana kuguswa na neema ya pekee kutoka kwa Mungu.

Maajabu ya Utoto na Jina la “Bonaventura”

Alipofikia umri wa miaka minne, Yohane alipata ugonjwa mkali uliomtishia maisha. Mama
yake, akiwa na hofu kubwa, alimkimbilia Mtakatifu Fransisko wa Asizi ili
amwombee mwanawe. Akamwekea nadhiri kwa Mungu kuwa akipona, atamtolea katika
maisha ya kitawa ya Wafranciskani. Mtakatifu Fransisko alisali, na mtoto
akapona.

Miaka kadhaa baadaye, Fransisko alipita tena katika mkoa huo, akakutana na mtoto
aliyemwombea zamani. Alipomshika mikononi mwake kwa furaha, alitamka maneno ya
ajabu: “O buona ventura!” – yaani “Ee bahati njema!” Tangu hapo, Yohane akaanza
kujulikana kwa jina hilo – Bonaventura.

Maisha ya Kitawa na Masomo

Bonaventura alitimiza ahadi ya mama yake. Akiwa na umri wa miaka 21, aliingia rasmi katika
Shirika la Wafranciskani. Baada ya kutoa nadhiri, alipelekwa kusomea falsafa na
teolojia katika Chuo Kikuu cha Paris, Ufaransa.

Katika Paris, aliendelea na masomo yake chini ya John wa Rochelle, na hapo ndipo
alipokutana na rafiki yake mkubwa Mtakatifu Thomas wa Akwino. Wote wawili
walipata shahada ya udaktari wa teolojia, na wakawa watu wa heshima katika
elimu ya kanisa. Walikuwa pia karibu na Mfalme Louis wa Ufaransa.

Maisha ya Huduma na Uongozi

Alipofikisha miaka 35, Bonaventura alichaguliwa kuongoza shirika la Wafranciskani nchini
Ufaransa, wakati ambao kulikuwa na migawanyiko mingi. Kwa hekima yake,
alifanikiwa kurudisha umoja na amani. Alisimamia pia tafsiri ya maandiko ya
Mtakatifu Antony wa Padua.

Alikuwa mwandishi hodari wa vitabu vya falsafa na teolojia, na mafundisho yake
yaliwasaidia wengi kuelewa vizuri imani ya Kikristo.

Tofauti na Unyenyekevu wa Maisha

Ingawa alikuwa na hekima na elimu kubwa, Bonaventura aliishi maisha ya unyenyekevu wa
kushangaza. Papa Clement IV alipomteua kuwa Askofu wa York, Bonaventura aliomba
kwa unyenyekevu asiweko katika nafasi hiyo.

Lakini baadaye, Papa Gregory X alipomteua kuwa Askofu wa Albano na mmoja wa washauri
sita wa Papa, alikubali kwa moyo wa utiifu. Alikubali pia kuacha nafasi ya
kuongoza shirika lake, akijitoa kwa kazi mpya ya Kanisa kwa upendo.

Hadithi maarufu inasimulia kuwa wakati wajumbe wa Papa walipomletea kofia ya
Ukardinali, walimkuta akiosha sahani jikoni. Aliwaambia waiweke kofia hiyo juu
ya mti, kwa kuwa mikono yake ilikuwa imelowa mafuta. Alijua vyeo havimfanyi mtu
kuwa mkubwa, bali moyo wa huduma.

Kifo na Utakatifu

Mtakatifu Bonaventura alihudhuria Mtaguso Mkuu wa Pili wa Lyon mwaka 1274, ambako
alijitahidi kupatanisha Kanisa la Magharibi (la Roma) na Kanisa la Mashariki
(la Kigiriki). Huko ndiko alipofariki tarehe 15 Julai 1274, akazikwa mjini
Lioni, Ufaransa.

Alitangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Sixtus IV mwaka 1482, na baadaye kutangazwa kuwa Mwalimu
wa Kanisa mwaka 1588.

Nukuu Maarufu ya Mtakatifu Bonaventura

Mtakatifu Toma wa Akwino alimtembelea siku moja na kumuuliza: “Umejifunza wapi mafundisho
yako yote?” Bonaventura akamwonyesha msalaba uliokuwa mezani na kusema, “Msalaba
huu ndiyo kitabu changu bora. Nimejifunza zaidi kwa kusali mbele ya Msalaba
kuliko kwa kusoma vitabu.”

Watakatifu Wengine wa Tarehe 15 Julai

  • Mt. Abudimus
  • Bl. Alphonsus de Vaena
  • Mt. Andrew Nam-Thuong
  • Bl. Anne Jahouvey
  • Bl. Anthony Francisco
  • Mt. Apronia
  • Mt. Athanasius
  • Mt. Baldwin
  • Mt. Benedict
  • Mt. Catulinus
  • Mt. David wa Sweden
  • Mt. Donald wa Ogilvy
  • Mt. Edith wa Polesworth
  • Mt. Egino
  • Mt. Esternus
  • Mt. Eutropius
  • Mt. Jacob wa Nisibis
  • Bl. James Andrade
  • Bl. Joanninus de San Juan
  • Bl. John Fernandez
  • Bl. Mark Caldeira
  • Bl. Nicholas Dinnis
  • Bl. Peter Berna
  • Mt. Peter Tuan
  • Mt. Philip
  • Mt. Plechelm
  • Mt. Pompeius Maria Pirotti
  • Wt. Secundinus, Agrippinus, Maximus, Fortunatus, na Martialis
  • Mt. Seduinus
  • Mt. Swithun
  • Mt. Vladimir

Mtakatifu Bonaventura, Wenyeheri na Watakatifu wengine wote wa leo, mtuombee.